USAWIRI WA MOTIFU ZA KIMAZINGIRA KATIKA TAMTHILIA YA KISWAHILI: TATHMINI YA MAJIRA YA UTASA (AREGE, 2015)
Abstract
Suala la kuongezeka kwa viwango vya halijoto na mabadiliko ya angahewa limeibua mijadala katika kiwango cha
kitaifa na kimataifa. Kwa msingi huu, kazi mbalimbali za kifasihi zimebuniwa kwa kuangazia uharibifu wa
mazingira asilia na athari zake na mwito wa kuhifadhi mazingira. Makala hii ilikusudia kuchunguza jinsi motifu za
kimazingira zilivyosawiriwa katika tamthilia ya Majira ya Utasa (Arege, 2015). Msisitizo ulikuwa kuangazia jinsi
mwandishi wa Majira ya Utasa amesawiri motifu za kimazingira ili kuonyesha uharibifu wa mazingira pamoja na
matatizo yanayotokana na uharibifu huo. Hii ni kwa sababu fasihi huwasilisha hali, maingiliano na mikinzano
miongoni mwa binadamu na mazingira. Kwa hivyo, ni mojawapo ya nyenzo inayoweza kuchangia katika kuangazia
matatizo yanayokumba jamii yoyote iwayo. Makala hii iliongozwa na nadharia ya Uhakiki wa Kiekolojia
iliyoasisiwa na Glotferty (1996). Kimsingi, nadharia ya uhakiki wa kiekolojia hujikita katika uchambuzi wa kazi za
kifasihi kwa kuonyesha uhusiano na utegemeano baina ya binadamu na mazingira. Tamthilia ya Majira ya Utasa
iliteuliwa kimakusudi kwa kuwa maudhui yake makuu yanahusiana moja kwa moja na mada ya makala hii. Data
ilikusanywa kupitia usomaji wa kina wa tamthilia teule. Matokeo ya makala hii yalithibitisha kuwa mwandishi wa
tamthilia ya Majira ya Utasa amesawiri motifu za kimazingira kwa namna mbalimbali kwa kuonyesha njia za
uharibifu wa mazingira na athari zake. Hivyo, kushadidia kuwa fasihi inaakisi kikamilifu matatizo yanayoibuka
katika jamii ilimoibuka. Kwa hivyo, ni chombo madhubuti kinachoweza kutumiwa kutatua matatizo hayo.